Kitendo cha kutupa samaki kinaweza kuonekana kama kitendo kisicho cha kawaida au jambo lisilo la busara, lakini kwa ujumla huwepo upotevu mkubwa wa samaki baada ya kuvuliwa. Baadhi ya wavuvi hutupa samaki waliochina wakiwa ndio wanawatoa kwenye nyavu majini. Hata hivyo sehemu kubwa ya samaki waliovuliwa hupotea baada ya kumtoa samaki majini. Katika nchi zenye joto, samaki wanaanza kuharibika kwa haraka wakiwa bado kwenye boti au mtumbwi; ikiwa hawakuhifadhiwa kwa kutumia barafu au majokofu kabla ya kuchakatwa. Uharibifu huo kwa kiwango tofauti unaendelea katika maeneo ya kuuzia mialoni, wakati wa uchakataji, wakati wa kusafirisha kupeleka sokoni na wakati samaki wanasubiri mteja sokoni. Katika maeneo ya Afrika inakadiriwa kuwa samaki wanaoharibika kabla ya kumfikia mlaji ni kati ya asilimia ishirini na ishirini na tano, na wakati mwingine hufikia hadi asilimia hamsini. Kwa ujumla viwango hivi vya upotevu havikubaliki na hii si habari njema.
Upotevu wa samaki baada ya kuvuliwa kama ilivyoainishwa hapo juu hutokea katika hatua mbalimbali za mnyororo wa uchakataji kuanzia wakati wa kumvua samaki mpaka anapofika mezani mwa mlaji. Upotevu huu umekuwa ni changamoto ya kimaendeleo kwa jamii za wavuvi, wachakataji na wafanya biashara ya mazao ya samaki katika muktadha wa kuboresha maisha yao. Upotevu wa samaki, na hasa kwa wavuvi wadogo, ni wa juu sana na unasababishwa na changamoto nyingi za uchakataji, ikilinganishwa na upotevu unaotokea katika nyanja za uzalishaji wa vyakula vya aina nyingine.
Upotevu wa samaki unaelezewa kama virutubisho vya samaki au thamani yake, ambavyo vilikuwa na uwezo wa kumfikia mlaji lakini havimfikii kama bidhaa za asili. Upotevu wa samaki baada ya kuvuliwa unaweza kugawanywa tena katika maeneo makuu matatu; upotevu halisi wa samaki au sehemu ya samaki, upotevu wa ubora wa samaki na upotevu wa kibiashara. Upotevu halisi unaelezewa kama samaki wanaotupwa kwa bahati mbaya, kwa kukusudia, kwa kuamrishwa au kwa kuliwa na wadudu, ndege au wanyama. Upotevu wa ubora unahusishwa na mabadiliko yanayo sababishwa na kuharibika kwa kuchina kwa samaki mwenyewe au madhara kama ya kuvunjika kwa samaki wakati wa uchakataji au usafirishaji, japo hayasababishi samaki wasiuzwe hata kama ni kwa bei ya chini. Upotevu wa kibiashara ni upotevu unaosababishwa na nguvu za soko ambapo wauzaji wa samaki wanaweza kulazimika kuuza samaki wenye viwango vizuri vya ubora kwa bei ya chini kuliko matarajio yao.
Upotevu wote huu una madhara ya kifedha kwa mvuvi, mchuuzi na kwa uchumi wa taifa. Hata hivyo ili kutatua tatizo la upotevu huu njia mbali mbali zinatakiwa kutumika katika mnyororo huo wa uzalishaji mpaka zinapomfikia mlaji sokoni. Tatizo hili ni kubwa ikizingatiwa kuwa uzalishaji wa samaki wanaovuliwa unapungua siku hadi siku. Kwa kutambua hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (FAO), limetoa Waraka wa Kuzingatiwa wa Uvuvi Endelevu (Code of Conduct for Responsible Fisheries) unaosisitiza umuhimu wa kupunguza upotevu wa samaki.
Upotevu wa samaki nchini Tanzania unaosababishwa na upotevu uliotajwa, ukiacha ule wa kiuchumi, ni Shilingi za ki tanzania kati ya bilioni kumi na mbili na ishirini kwa uvuvi wa samaki aina ya dagaa kwa mwaka wa fedha 2005/06. Juhudi za kupunguza upotevu wa samaki baada ya mavuno ni muhimu ili kuongeza mapato na usalama wa chakula, bila kuongeza juhudi za uvuvi. Kwa nini kuongeza uvuvi zaidi wakati tunaweza kudhibiti kiasi cha samaki kilichovuliwa tayari kisipotee?
Kuboreshwa mbinu za uchakataji ni jibu kwa upotevu wa samaki unaotokea katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Kiwango cha wastani wa tani 30,000 huvuliwa kwa mwaka kutoka Ziwa Nyasa mwambao wa Tanzania. Upotevu wa samaki Ziwa Nyasa wakati mwingine na hasa wakati wa mvua hufikia hadi asilimia hamsini ya samaki waliovuliwa na hasa kwa samaki wadogo. Sehemu kubwa ya upotevu wa samaki baada ya kuvunwa hutokana na jamii za Usipa, Mantura, Ngelwa na Vitui. Upotevu hutokana na desturi za ukaushaji samaki kwa kutumia moshi au kwa kuanika mchangani.
Mbinu za gharama nafuu zimekuwa zikibuniwa na jamii nyingi za wavuvi, mara nyingi na wanawake, ambao ndio hasa hujishughulisha na ununuzi wa samaki wanaoletwa kwenye mialo. Samaki ni bidhaa muhimu ya chakula Tanzania na huvunwa kwa sehemu kubwa na wavuvi wadogo. Samaki ambaye hawezi kuuzwa akiwa mbichi lazima ahifadhiwe kwa kukaushwa kwa jua au moshi au kwa kuwekwa chumvi au kusindikwa kama ngo’nda. Kwa Kutambua haja ya upatikanaji wa mbinu ya ukaushaji wa samaki kwa kutumia tekinolojia nafuu na rafiki wa mazingira, TAFIRI kwa msaada wa fedha kutoka COSTECH imeboresha makaushio (dryers) ya gharama nafuu yanayotumia nishati ya jua kwa ajili ya ukaushaji wa samaki wadogo wadogo. Faida za kutumia makaushio ya nishati ya jua ni nyingi; chache kati ya hizo ni upatikanaji wa jua sehemu kubwa ya mwaka, ubora wa bidhaa zinazokaushwa kwa kutumia majiko haya, ukaushaji wa haraka kwani majiko haya yanahifadhi joto kubwa ukilinganisha na ukaushaji wa eneo la wazi na hivyo kuboresha kipato cha wavuvi wa bonde la ziwa Nyasa na maeneo mengine. Makaushio haya yanatarajiwa kupunguza hasara inayotokana na uharibikaji wa samaki baada ya mavuno na kuongeza ubora unaomfikia mlaji katika masoko lengwa. Mkakati huu unatarajiwa kuboresha usalama wa chakula na kipato cha wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara ya samaki katika mwambao wa ziwa Nyasa.
Mradi ulianza mwaka 2013 na lengo kuu la mradi likiwa ni kuboresha mbinu za matumizi ya nishati ya jua katika kukausha samaki kwa kutumia makaushio au majiko yanayotumia nishati ya jua. Majiko haya yamekusudiwa kutengenezwa kwa kutumia kadri iwezekanacyo vifaa vinavyopatikana kiurahisi katika mazingira husika. Makaushio yaliyochunguzwa ni aina nne, aina ya hema (tent), boksi (box), shimo (tunnel), na meza ya wazi (drying rack). Utendaji kazi wamakaushio haya kwa kuzingatia uwezo wa kuhifadhi joto na unyevu nje na ndani, kiwango cha mwendo kasi wa upepo wa nje, kasi ya ukaushaji na muda wa bidhaa kudumu bila kuharibika baada ya kukaushwa vilipimwa. Chumvi ili tumiwa kama kitunza ubora wa samaki. Sampuli za samaki wakavu waliochakatwa zilipelekwa kwenye maabara za Chuo Kikuu cha Sokoine ili kuchunguza viinilishe na madini (proximate analysis and minerals). Aina ya kaushio la hema linaonyesha kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na makaushio mengine bila kuzingatia ubora wa samaki waliokaushwa. Hii ni kwa sababu bado takwimu za ubora wa sampuli za samaki waliokaushwa na kupelekwa maabara kuchunguzwa hazijakamilika kuchakatwa.
Mradi utatekelezwa kwa awamu tatu kwa muda wa miaka minne. Awamu ya kwanza ilifanya maandalizi ya manunuzi ya vifaa na imefanya majaribio ya majiko ili kubaini jiko au kaushio bora zaidi na yanayofaa kwa kukaushia aina ya samaki lengwa katika mazingira halisi katika kijiji cha Matema kilichopo kaskazini kabisa mwa Ziwa Nyasa. Awamu ya pili itahusika na kusambaza takinolojia kwa walengwa, ambapo inakusudiwa kufanyika katika vijiji tisa katika wilaya tatu zilizopo kwenye mwambao wa ziwa Nyasa upande wa Tanzania. Eneo hilo lina tarafa zifuatazo: – Ntebela na Nyakyusa ( Kyela ), Mwambao na Masasi ( Ludewa ) na Ruhuhu na Luhekei ( Mbinga ). Sifa na vigezo vya kuchaguliwa kwa vijiji hivyo miongoni mwa zingine ni kwa kiasi gani maisha ya jamii ya wanakijiji hutegemea uvuvi, aina za samki zinazopatikana kwa mwaka mzima na umbali wa kijiji kutoka ziwani. Wakati wa kusambaza teknolojia litafanyika dodoso la kubaini hali halisi ya kijamii na kiuchumi ya jamii za wavuvi. Taarifa zitakazokusanywa zitasaidia kubaini mchango wa teknolojia hii katika maisha ya jamii ya wavuvi mwishoni mwa mradi. Awamu ya mwisho haitakamilika kwa kuanzisha na kusambaza majiko haya kwa wananchi tu, bali pia kutoa ripoti kamili ya ujumla ya mradi. Maandalizi kwa ajili ya ripoti hii ya yanaendelea. Mradi unatarajiwa kufika mwisho wake mwaka 2016 baada ya kufanya tathmini za kiuchumi jamii kubaini mafanikio ya matumizi ya teknolojia hii.