Ugonjwa ni nini? Ugonjwa ni mabadiliko kutoka katika afya ya kawaida ya mnyama/kuku. Hali hii hutokea pale

vimelea au vijidudu vinapoingia mwili wa mnyama, kwa kula vyakula vyenye sumu, au inapotokea kuna uhaba wa lishe au madini mwilini.
 
TOFAUTI ZA MUONEKANO KATI YA KUKU MWENYE AFYA NA KUKU MGONJWA
KUKU MWENYE AFYA NZURI
Ø  Macho na sura angavu
Ø  Hupenda kula na kunywa maji
Ø  Pua zilizo safi, upanga na undu mwekundu, manyoya
laini na yaliyopangika vizuri
Ø  Hupumua kwa utulivu
Ø  Sehemu ya kutolea haja huwa kavu
Ø  Kinyesi kikavu, cheupe na kisicho na rangi
Ø  Hutaga mayai kawaida
KUKU ASIYE NA AFYA NZURI
Ø  Huonekana mchovu na dhaifu
Ø  Hula na kunywa kidogo au zaidi ya kawaida
Ø  Hutoa kamasi puani, ute na matongotongo; manyoya
yaliyovurugika
Ø  Hupumua kwa shida na kwa sauti
Ø  Sehemu ya kutolea haja inakuwa na unyevunyevu na
kinyesi kuganda
Ø  Huharisha, kinyesi huwa na damu au minyoo
Ø  Hutaga mayai machache au husimama kutaga kabisa
Ø  Huwa na tabia ya kujitenga na wenzake katika kundi
MGONJWA MUHIMU YANAYOSABABISHWA NA BACTERIA
HOMA KALI YA MATUMBO (FOWL TYPHOID)
Maelezo: Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bacteria na hushambulia zaidi kuku
Wakubwa pia na vifaranga. Ugonjwa pia hushambulia aina zote za bata, kanga na ndege
wa porini.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea: Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa
na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza
ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika. Pia mashine za kutotolea zilizochafuliwa zinaweza kuambukiza vifaranga.
Dalili
Kuku wakubwa
Ø  Kuharisha kinyesi cha majimaji na cha rangi ya njano
Ø  Vifo vya ghafla
Ø  Kupauka kwa upanga na masikio kwa sababu ya kupungukiwa damu
Ø  Manyoya hutimka, hushusha mbawa, hufumba macho na kuzubaa (kuvaa koti)
Vifaranga
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au dhaifu
Ø  Hujikusanya pamoja na kukosa hamu ya kula
Ø  Kinyesi cha rangi ya njano na huganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Hupumua kwa haraka na kwa shida
Ø  Vifo vingi huweza kutokea kuku wasipotibiwa
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Kinyesi cha rangi ya njano na kijani kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja kubwa
Ø  Misuli iliyovia na damu kuwa nyeusi
Ø  Ini lililovimba na kuwa na rangi ya pinki
Ø  Bandama lililovimba
Ø  Figo na mayai yaliyovia
Ø  Mabaka meupe kwenye sehemu ya juu ya figo
Tiba
v  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa.
Lakini madawa haya hayawezi kumaliza kabisa ugonjwa kutoka shambani.
v  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika mashamba ambayo hayana huu ugonjwa
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wako mara kwa mara na kuondoa/kuchinja kuku
wanaonyesha dalili za ugonjwa.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani.
Ø  Fanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi ya kuku kwa kutumia
viuatilifu vilivyopendekezwa.
Aina nyingine ya Homa ya Matumbo (Avian Paratyphoid) inafanana na aina iliyoelezwa hapo juu, tofauti kubwa
ni aina ya vimelea vinavyosababisha aina hii ya homa, na huathiri zaidi kuku na bata wadogo.
HOMA YA MATUMBO (AVIAN PARATYPHOID)
Maelezo: Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bakteria wa spishi tofauti na ya bakteria wanaosababisha homa
kali ya matumbo na hushambulia zaidi kuku na bata wadogo. Vimelea vya ugonjwa huu huweza kusababisha homa ya matumbo kwenye binadamu.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, mbwa,
Ø  ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa
Ø  ugonjwa na kuchafua vyanzo vya maji na vyakula.
Ø  Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika. Pia mashine za kutotolea zilizochafuliwa zinaweza kuambukiza vifaranga.
Dalili
Vifaranga
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au mara tu baada ya kuanguliwa
Ø  Hujikusanya pamoja karibu na joto
Ø  Uharo kuganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Vifo kwenye vifaranga vinaweza kufikia hadi asilimia 50.
Kuku wakubwa
Ø  Vifo vya ghafla Kuharisha kinyesi cha majimaji na cha rangi ya njano
Ø  Kuku kuharisha
Ø  Kupungua kwa uzito
Ø  Kuku wa mayai hupunguza utagaji
Ø  Kuku anaonekana mchovu
Uchunguzi wa Mzoga
Mabadiliko muhimu katika mzoga wa kifaranga ni:
Ø  Ini kuvimba na kuvia
Ø  Uvimbe mweupe mdogo mdogo kwenye ini
Ø  Mapafu kuvia
Ø  Utumbo kuvimba
Ø  Njano ya yai kutapakaa tumboni
Tiba
Ø  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki na sulfa ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na
ugonjwa. Lakini madawa haya hayawezi kumaliza kabisa ugonjwa kutoka shambani.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika mashamba ambayo hayana huu ugonjwa.
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wako mara kwa mara na kuondoa/kuchinja kuku
wanaonyesha dalili za ugonjwa.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani.
Ø  Fanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi ya kuku kwa kutumia
viuatilifu vilivyopendekezwa.
Ø  Mayai yakusanywe mara kwa mara
Ø  Hakikisha vifaranga wanapata joto la kutosha.
KUHARISHA KINYESI CHEUPE (BACILLARY WHITE DIARRHEA)
Maelezo
Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bakteria na hushambulia zaidi kuku wadogo wenye umri hadi wiki tatu. Ugonjwa pia hushambulia aina zote za bata, kanga na ndege wa porini (mbuni).
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku iliyokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Ø  Kuku waliopona baada ya matibabu wanaweza kuendelea kuchafua mazingira na kuwa chanzo cha
maambukizi, hivyo waondolewe shambani.
Ø  Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika.
Tahadhari: Wageni na wafanyakazi wanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba hadi shamba au
banda hadi banda.
Ø  Vituo vya kutotolea vifaranga vinaweza kuwa chanzo. Hakikisha vifaranga wako hawatoki kwenye kituo chenye kuku wagonjwa.
Dalili
Vifaranga
Ø  Vifo vya ghafla
Ø  Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au dhaifu
Ø  Hujikusanya pamoja karibu na taa kwa ajili ya kupata joto
Ø  Uharo wa rangi nyeupe kama chaki
Ø  Hupumua kwa shida
Ø  Uharo huganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Ø  Vifaranga wanapiga sana kelele
Ø  Vifaranga wanaonyesha ulemavu
Ø  Kuvimba magoti
Kuku wakubwa
Ø  Kuku wakubwa huonyesha dalili za ugonjwa sugu
Ø  Kupauka kwa upanga na masikio kwa sababu ya kupungukiwa damu
Ø  Utagaji wa mayai hupungua
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Njano ya yai iliyotapakaa tumboni mwa kuku
Ø  Uvimbe mdogo mdogo wa rangi ya kijivu ulioenea kwenye moyo,firigisi, misuli, mapafu na sehemu ya nje ya utumbo katika kuku wakubwa (umri wa wiki 2 hadi 5)
Tiba
Ø  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki ambayo yanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa.
Ø  Lakini madawa haya hayawezi kumaliza ugonjwa shambani kabisa.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika vyanzo vilivyothibitishwa kuwa havina huu ugonjwa
Ø  Tengeneza utaratibu wa kufanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi
ya kuku kwa kutumia viuatilifu vilivyopendekezwa.
Ø  Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wote wenye umri zaidi ya miezi mitano (5) mpaka hapo
kundi lote litakapoonyesha kwamba hakuna kuku mwenye maambukizi, kuku salama wahamishiwe
katika mabanda safi.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani au bandani.
KIPINDUPINDU CHA KUKU (FOWL CHOLERA)
MAELEZO
   Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bacteria ambao huenea kwa haraka na kusababisha vifo vingi. Ugonjwa hushambulia kuku na ndege wa aina zote ijapokuwa jamii ya bata huathirika zaidi kuliko kuku.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni hewa, maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa.
Ø  Kwa kawaida ugonjwa huanza kwa kuingiza katika shamba/banda kuku wagonjwa kutoka nje. Baada ya
vimelea kuingia huenea kwa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa.
Ø  Udongo uliochafuliwa na kinyesi cha kuku mgonjwa huweza kuchafua maji na vyakula
Ø  Hewa kutoka kwa kuku wagonjwa inaweza kuwa chanzo cha maambukizi.
Ø  Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Dalili
Kuku wanaweza wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa, lakini dalili zifuatazo zinaweza kuonekana:
Ø  Vifo vya ghafla vya idadi kubwa ya kuku waliokuwa na afya
Ø  Kuku wanakonda
Ø  Kuku wanapumua kwa shida, wanakohoa na kupiga chafya
Ø  Uharo wa rangi ya kijivu, njano au kijani na unaonuka
Ø  Vifaranga wanaonyesha ulemavu
Ø  Kuvimba magoti na kifundo cha mbawa
Ø  Kichwa, upanga na undu hugeuka kuwa rangi nyeusi au zambarau
Ø  Vifo vya kuku vinaweza kufikia asilimia 20
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Madoa ya damu kwenye mapafu, utumbo na kuzunguka moyo.
Ø  Ini huvimba, laini na kuonekana kama limepikwa.
Ø  Uchafu mgumu uliogandamana katika eneo linalozunguka utumbo, kwenye masikio na machoni
Ø  Pua na mdomo kuwa na makamasi mazito na machafu
Tiba
v  Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki na sulfa ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tiba na kinga.
v  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Utaratibu ulio mzuri zaidi ni kuondoa kuku wote kutoka kwenye shamba/banda ambalo ugonjwa
umethibitishwa, kupuliza dawa za viuatilifu kabla ya kuingiza vifaranga na kuku wapya
Ø  Mabanda yote ya kuku yapuliziwe dawa za viuatilifu kabla ya kuingiza kuku wapya.
Kuku wapya watenganishwe na kuchunguzwa kwa muda wa angalau mwezi mmoja kabla ya
kuwachanganya na kuku wengine.
Ø  Vifaranga visichanganywe na kuku wakubwa.
Ø  Hakikisha unafuata kanuni za ufugaji bora ili kuku wakue vizuri na wasiathirike
MAFUA YA KUKU (INFECTIOUS CORYZA )
Maelezo
   Ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria ambao hushambulia zaidi kuku na ndege wa porini. Ugonjwa
hushambulia kuku wa umri wowote.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa.
Ø  Kuku au ndege wagonjwa huambukiza wenzao kupitia mfumo wa hewa wanapopiga chafya.
Dalili
Ugonjwa huu hushambulia zaidi mfumo wa hewa na hivyo kusababisha dalili zifuatazo:
Ø  Makamasi mazito yenye usaha hutoka puani
Ø  Kuku anashindwa kupumua, hukohoa na kupiga chafya
Ø  Harufu mbaya kutoka kinywani na machoni
Ø  Uso mzima unavimba pamoja na upanga
Ø  Vifo vya kuku vinaweza kufikia asilimia 20
Tiba
Ø  Madawa aina ya sulfa na antibiotiki yanaweza kutumika kwa ajili ya tiba na kinga.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Iwapo ndani ya shamba moja kuna kuku wa aina tofauti, k.m. vifaranga, kuku wazazi, kuku wakubwa,
jaribu kuwatenganisha ili mabanda yao yasikaribiane
Ø  Pale inapowezekana, jaribu kupanga utaratibu wa kila kundi la kuku lishughulikiwe na mfanyakazi wake ili kuzuia kueneza maambukizi.
Ø  Hakikisha kuku wagonjwa wanatengwa na wale wazima
Ø  Tumia maji yaliyowekwa dawa aina ya klorini
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi
shambani.
UGONJWA SUGU WA MFUMO WA HEWA
(CHRONIC RESPIRATORY DISEASE-CRD)
MAELEZO
Ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria ambao hushambulia zaidi kuku na bata mzinga.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa na wenye
Vimelea. Pia kupitia mfumo wa hewa kutoka ndege wagonjwa.
Ø  Njia kuu ya kuenea kwa maambukizi ni kupitia mayai, hivyo maambukizi huendelea kutoka kizazi hadi
Kizazi.
Ø  Tahadhari: Wageni, wafanyakazi na magari yanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba hadi shamba au banda hadi banda
Dalili
Ugonjwa huu hushambulia zaidi mfumo wa hewa na hivyo kusababisha dalili zifuatazo:
Ø  Kuku hukoroma
Ø  Kuku hutoa makamasi
Ø  Kuku wanakohoa kwa muda mrefu, wiki hadi miezi
Ø  Kuvimba macho
Ø  Kutingisha kichwa
Ø  Vifo vya kuku vinaweza kufikia hadi asilimia 20
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Athari kubwa za ugonjwa huu ni kwenye mfumo wa hewa, hivyo mabadiliko yanakuwa katika mfumo
mzima wa hewa.
Ø  Kamasi nzito zenye usaha zilizotapakaa kwenye pua, koromeo, mapafu na vifuko vya hewa
Tiba
Ø  Madawa aina ya sulfa na antibiotiki yanaweza kutumika kwa ajili ya tiba na kinga.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi na watu wengine wanazuiwa kuranda randa kutoka banda
hadi banda. Ikiwa lazima kufanya hivyo, basi pawepo utaratibu wa kuoga na kubadilisha nguo kati ya
banda moja kwenda jingine.
Ø  Epuka kuingiza kuku wagonjwa katika shamba/banda ambalo halina ugonjwa
Ø  Hakikisha mabanda yana joto linalostahili na mzunguko wa hewa mzuri, pia kuku wapewe chakula cha Kutosha
KOLIBASILOSI (COLIBACILLOSIS)
Maelezo
  Ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria na hushambulia zaidi kuku na bata. Ugonjwa huu huathiri zaidi vifaranga.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Bakteria
Wanaosababisha ugonjwa wameenea kila mahali hivyo kuweza kuchafua maji na chakula.
Ø  Vifaranga wanaweza kupata maambukizi wakiwa bado ndani ya yai kabla ya kuanguliwa.
Ø  Mayai machafu yenye bacteria ndiyo njia kuu ya kuambukiza vifaranga kupitia kitovu baada ya
kutotolewa. Pia mayai yenye maganda dhaifu na makasha machafu ya kubebea mayai ni chanzo kingine
cha maambukizi.
Dalili
Ø  Kuku wanaonekana kuzubaa
Ø  Kuku wanatoa sauti ya chini chini
Ø  Kuku wanajikusanya karibu na taa inayotoa joto
Ø  Kuharisha na kinyesi kugandana katika njia ya haja
Ø  Ngozi ya kifuani ina uvimbe
Ø  Vifo vya vifaranga vinaweza kufikia asilimia 10, vifaranga walio totolewa inaweza kufika asilimia 50.
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Sehemu ya haja inaweza kuzibwa na kinyesi kilichokauka
Ø  Njano ya yai kutapakaa tumboni, uchafu wenye rangi nyeupe au kijani, ukiwa na damu Uvimbe kwenye ini, utumbo na utandu wa tumboni
Tiba
Ø  Madawa aina ya sulfa na antibiotiki yanayofaa yanaweza kutumika kwa ajili ya tiba na kinga.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Angamiza kwa kuchoma moto vifaranga wote ambao hawakui vizuri na wanaonyesha dalili za ugonjwa
Ø  Mabanda yote ya kuku yapuliziwe dawa za viuatilifu kabla ya kuingiza kuku na vifaranga wapya.
MAGONJWA MUHIMU YA VIRUSI
Mdondo/Kideri, Gumboro, Mareksi, Ndui ya Kuku, Mafua Makali ya Ndege na Ugonjwa Unaoathiri Mfumo wa Fahamu.
MDONDO/KIDERI (NEWCASTLE DISEASE)
Maelezo
   Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia aina zote za spishi za ndege, ijapokuwa kuku ndio aina inayoathirika zaidi. Binadamu na wanyama wengine pia wanaweza kuambukizwa. Ugonjwa huathiri mifumo ya fahamu, njia ya chakula na hewa.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni maji, chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Pia maambukuzi huweza kupitia mfumo wa hewa kutoka kwa kuku wagonjwa.
Ø  Kuku, vifaa vya kazi na bidhaa zitokanazo na kuku (nyama, mayai, manyoya na mbolea) kutoka mashamba yenye ugonjwa zinaweza kueneza ugonjwa kutoka shamba moja hadi jingine.
Ø  Vifaranga wanaweza kupata maambukizi kutoka vituo vya kutotolea vifaranga kutokana na maganda ya
mayai yaliyochafuliwa.
Dalili
Ø  Vifo vya ghafla vya idadi kubwa ya kuku katika shamba/banda
Ø  Kuku wanatetemeka na kushindwa kutembea
Ø  Kuku hupooza miguu, mabawa na kupinda shingo; na hujizungusha mahali alipo
Ø  Kuku huharisha kinyesi cha kijani na wakati mwingine chenye mchanganyiko wa rangi ya njano
Ø  Kuku huzubaa na kuacha kula
Ø  Kuku hukohoa, hupiga chafya na kupumua kwa shida
Ø  Vifo vinaweza kufikia asilimia 100, kutegemea na umri na aina ya ndege
Uchunguzi wa Mzoga
Ugonjwa huathiri zaidi mfumo wa hewa na njia ya chakula, hivyo mabadiliko yanayoonekana kwenye mzoga ni pamoja na:
Ø  Madoa ya damu kwenye mfumo wa hewa
Ø  Kamasi nzito zenye rangi ya njano kwenye koromeo
Ø  Utandu mweupe kwenye mifuko ya hewa
Ø  Bandama kuvimba
Ø  Uvimbe kwenye kichwa na eneo la shingo
Ø  Madoa madogo madogo ya damu kwenye kifua, mafuta na utandu wa tumboni
Ø  Damu kuvia kwenye mfumo wa usagaji chakula – juju, firigisi, tumbo na utumbo
Tiba
Ø  Hakuna tiba ya ugonjwa huu ila kuku wapewe antibiotiki.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege hawaingii hovyo kwenye shamba/banda
Ø  Angamiza mizoga yote kwa njia stahiki kwa kuchoma moto au kufukia kwenye shimo refu ardhini.
Ø  Hakikisha banda la kuku lina hewa ya kutosha na epuka msongamano mkubwa wa kuku.
Ø  Fanya usafi wa mara kwa mara kwenye vyombo vya kuwekea maji na chakula, pamoja na mabanda ya kuku.
Ø  Zuia uingizaji holela wa kuku wageni wasiochanjwa kwenye shamba/banda. Kuku wanaoingia shambani/ bandani watoke maeneo yasiyokuwa na ugonjwa.
Ø  Tenganisha kuku kufuatana na umri
Ø  Maeneo yenye ugonjwa yawekwe chini ya karantini na mabanda yapulizwe dawa
Ø  Kuku wapewe Chanjo tangu vifaranga wa umri wa siku 3, baada ya wiki 3 – 4, na baadaye kila baada ya miezi 3.
Gumboro (Infectious Bursar Disease)
Maelezo
  Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia zaidi kuku, bata maji na bata mzinga. Kuku na bata wadogo hadi wiki 12 ndio wanaoathirika zaidi.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Chanzo cha maambukizi ni maji, chakula na vifaa/vyombo vya shambani vilivyochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa na wenye vimelea.
Ø  Maambukizi pia huenea kupitia mfumo wa hewa, kwa vumbi lenye vimelea katika mabanda.
Chukua Tahadhari: Wageni, wafanyakazi na magari yanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba
hadi shamba au banda hadi banda. Hii ni pamoja na kuku hai, vifaa/vyombo vya shambani na bidhaa
zitokanazo na kuku (mayai, nyama, manyoya na mbolea) wanaosafirishwa kutoka mashamba/mabanda
yenye ugonjwa.
Dalili
Ø  Uharo mweupe wenye maji maji
Ø  Kuku wanadonoana kwenye sehemu ya kupitishia haja, na sehemu hii huvimba
Ø  Kuku hulala kifudifudi
Ø  Kuku wanashindwa kutembea na wanatetemeka
Ø  Vifo vya kuku vinaweza kufikia hadi asilimia 30, na kupungua jinsi wanavyozeeka
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Sudi (mkia) ya kuku huvimba mara mbili ya kawaida na kujaa maji.
Ø  Madoa ya damu kwenye miguu na mapaja.
Tiba
Ø  Hakuna tiba maalum
Ø  Kuku wapewe vitamini na maji kwa wingi
Ø  Antibiotiki husaidia maambukizi nyemelezi.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Mizoga, makapi na vifaa vingine vilivyochafuliwa na kuku wagonjwa vichomwe moto au kuzikwa.
Ø  Weka utaratibu madhubuti wa kupuliza dawa za viuatilifu vinavyofaa
Ø  Baada ya kumaliza kuwauza kuku wote, fanya usafi wa mabanda na kupuliza dawa
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege hawaingii hovyo kwenye shamba/banda
Ø  Kuku wapatiwe Chanjo katika maji ya kunywa (angalia Ratiba)
MAREKSI (MAREK’S DISEASE)
Maelezo
    Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia zaidi kuku, bata maji na bata mzinga. Kuku wa mayai ndio wanaoathirika zaidi. Mara nyingi ugonjwa hutokea katika kuku wenye umri kati ya wiki 12 hadi 24, ijapokuwa hata kuku wakubwa nao hupata ugonjwa.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Maambukizi pia kuenea kupitia mfumo wa hewa, kwa vumbi lenye vimelea katika mabanda na vumbi
litokanalo na manyoya.
Ø  Mate ya kuku wagonjwa pia ni njia mojawapo ya maambukizi
Ø  Binadamu, inzi na aina nyingine za ndege pia zinaweza kusambaza maambukizi.
Dalili
Ø  Uharo mweupe wenye maji maji
Ø  Mboni ya jicho kuwa na rangi ya kijivu
Ø  Upofu kwenye kuku
Ø  Miguu na mabawa hupooza
Ø  Kuku kupindisha kichwa
Ø  Kwa kawaida vifo ni kati ya asilimia 10 na 80.
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Uvimbe mweupe karibu katika viungo vyote laini vya mwili: maini, figo, bandama na ngozi.
Ø  Mishipa ya fahamu kuvimba katika miguu na mbawa zilizopooza
Tiba
Ø  Hakuna tiba maalum
Ø  Pata ushauri wa daktari
Kuzuia na Kinga
Ø  Mizoga, makapi na vifaa vingine vilivyochafuliwa na kuku wagonjwa vichomwe moto au kuzikwa.
Ø  Weka utaratibu madhubuti wa kupuliza dawa za viuatilifu vinavyofaa
Ø  Baada ya kumaliza kuwauza kuku wote, fanya usafi wa mabanda na kupuliza dawa
Ø  Hakikisha unatenganisha kuku wadogo na wakubwa hadi miezi 3, na watenganishe kuku kwa umri
Ø  Vifaranga vya siku moja vipatiwe Chanjo dhidi ya ugonjwa (angalia Ratiba)
NDUI YA KUKU (FOWL POX)
Maelezo
   Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambavyo hushambulia zaidi kuku, jamii ya bata na aina nyingi ya ndege pori. Kuku na ndege wa umri tofauti wote huweza kushambuliwa na sehemu zinazoathirika zaidi ni zile zisizo na manyoya. Virusi vinaweza kuishi katika mazingira kwa muda mrefu.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni vifaa/vyombo vya shambani vilivyochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa na wenye vimelea.
Ø  Maambukizi pia kuenea kupitia wadudu wanaouma kama chawa, kupe, nzi weusi na mbu.
Ø  Maambukizi pia kuenea kupitia majeraha wanayoyapata kuku wanapopigana na kukwaruzana au kugusana
Ø  Maambukizi kupitia mfumo wa hewa na chakula
Dalili
Ø  Ugonjwa unapoathiri ngozi hutokea vidutu vikubwa vya rangi ya kijivu au kahawia kwenye upanga, undu, macho na mdomoni
Ø  Ugonjwa unapoathiri sehemu laini za mwili, mabaka
madogo meupe hutokea kwenye kona za mdomo, kuzunguka ulimi, ndani ya mdomo na kwenye koo
Tiba
Ø  Hakuna tiba
Ø  Kuku wanaweza kupewa vitamini na glucose kupunguza makali ya ugonjwa
Ø  Antibiotiki na maji yenye chumvi husaidia maambukizi nyemelezi.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Kuku wote walioathirika waondolewe shambani/bandani.
Ø  Mizoga, makapi na vifaa vingine vilivyochafuliwa na kuku wagonjwa vichomwe moto au kuzikwa.
Ø  Pulizia kemikali za kuua wadudu
Ø  Weka utaratibu madhubuti wa kupuliza dawa za viuatilifu vinavyofaa japokuwa inawezekana visiuwe
virusi wote
Ø  Kuku wapatiwe Chanjo wakiwa na wiki 6. Maeneo mengine chanjo inatakiwa kufanywa mapema zaidi. (Angalia Ratiba).
MAFUA MAKALI YA NDEGE (HIGHLYPATHOGENIC AVIAN INFLUENZA )
Maelezo
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao hushambulia aina zote za ndege pamoja na binadamu.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Chanzo cha maambukizi ni mayai yaliyoambukizwa, ndege wagonjwa na mashine za kutotolea
Ø  Zilizochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa na wenye vimelea.
Ø  Maambukizi huenea kupitia maji maji ya kuku wagonjwa, kinyesi, vifaa na nguo za wafanyakazi na maji ya kunywa.
Ø  Mayai yaliyoambukizwa yakipasuka katika mashine za kutotolea yanaweza kuambukiza vifaranga na
Ø  kufanana na maambukizi yanayotoka kizazi kimoja hadi kingine
Dalili
Ø  Vifo vya ghafla
Ø  Kelele za kawaida za kuku hazisikiki tena
Ø  Kuku hukohoa
Ø  Pua kutoa makamasi na macho machozi
Ø  Kuvimba kwa uso
Ø  Upanga na undu zinakuwa na rangi ya bluu
Ø  Uharo (mara nyingi wa rangi ya kijani)
Ø  Dalili za kuathirika mfumo wa fahamu, kama vile kupooza
Ø  Kuku wengi huambukizwa lakini vifo ni vichache, asilimia 5 hadi 50.
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Uharo wenye damu.
Ø  Njia ya hewa kuvimba – pua, koromeo, mifuko ya hewa pamoja na utandu wa macho
Ø  Ovari zinakuwa na madoa ya damu na kupungua ukubwa
Ø  Upanga na undu zinakuwa na rangi ya bluu
Ø  Kichwa na shingo kuvimba
Ø  Mzoga unaonekana umekauka
Ø  Misuli imevia
Ø  Madoa ya damu kwenye firigisi na mafindofindo ya tumboni
Tiba
Ø  Hakuna tiba maalum
Ø  Pata ushauri wa daktari
Kuzuia na Kinga
Ø  Mizoga, ndege wagonjwa, makapi na vifaa vingine vilivyochafuliwa na kuku wagonjwa vichomwe moto
au kuzikwa.
Ø  Weka utaratibu madhubuti wa kupuliza dawa za viuatilifu vinavyofaa kwenye mabanda na vyombo
Ø  Baada ya kumaliza kuwauza kuku wote, fanya usafi wa mabanda na kupuliza dawa
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege kutoka kwa majirani hawaingii ovyo
kwenye shamba/banda
Ø  Kuku wanaotoka nje ya shamba wawekwe kwenye karantini kabla ya kuingizwa shambani/bandani
Ø  Zuia ndege wa porini wasiingie kwenye mabanda
MAGONJWA MUHIMU YA PROTOZOA
Maelezo
  Protozo ni vimelea vyenye chembe moja ambavyo husababisha magonjwa kwenye ndege na wanyama.
Mazingira ya joto na unyenvuyevu husababisha kuongezeka kwa Protozoa. Maambukizi mengi ni kwa njia ya kinyesi cha ndege wagonjwa kuchafua maji na chakula, nguo na viatu vya wafanyakazi, pamoja na nzi na wadudu wengine. Magonjwa muhimu yanayosababishwa na protozoa kwenye kuku nchini Tanzania ni: Kuhara Damu na Histomonasi.
KUHARA DAMU (COCCIDIOSIS)
Maelezo
   Ni ugonjwa unaosababishwa na Protozoa ambao hushambulia kuku na wanyama wengine. Ugonjwa huathiri kuku wadogo na wakubwa.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Maambukizi huenea kupitia kinyesi cha kuku wagonjwa kuchafua maji na chakula, udongo na maranda.
Ø  Njia kuu ya maambukizi ni kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na vimelea
Ø  Maambukizi yanaweza pia kupitia vifaa na vyombo vya shambani, nguo, wadudu na wanyama.
Dalili
Ø  Kuhara damu
Ø  Mbawa kushuka
Ø  Kuzubaa na kuacha kutaga
Ø  Kukosa hamu ya kula
Ø  Kupunguza kasi ya ukuaji na uzito
Ø  Kwa kawaida vifo ni vingi
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Njia ya haja kujaa damu
Ø  Madoa ya damu kwenye utumbo
Ø  Madoa madogo ya rangi nyeupe na nyekundu sehemu ya nje ya utumbo
Ø  Madoa ya rangi ya kijivu sehemu ya ndani ya utumbo
Ø  Utumbo mkubwa mpaka sehemu ya kutolea haja imevimba na kuwa ngumu
Ø  Sehemu ya chini ya utumbo mdogo imevimba na kuwa ngumu
Ø  Utumbo kujaa uchafu wa rangi ya kijivu na kahawia
Tiba
Ø  Amprolium hydrochloride
Ø  Sulfa
Ø  Pata ushauri wa daktari
Kuzuia na Kinga
Ø  Maranda na aina nyingine za malalo yawe makavu wakati wote.
Ø  Fuga kuku kwenye mabanda yenye sakafu isiyo na matundu
Ø  Vyombo vya chakula na maji visiwekwe chini, vining’inie juu ya sakafu kuzuia kuchafuliwa na kinyesi
Ø  Banda lisiwe na msongamano mkubwa wa kuku
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege hawaingii hovyo kwenye shamba/banda
Ø  Angamiza mizoga yote kwa njia stahiki kwa kuchoma moto au kufukia kwenye shimo refu ardhini. Pia na maranda na vifaa vilivyochafuliwa vichomwe.
Ø  Kutumia dawa za tiba kwa ajili ya kinga. Hii ifanyike kwa muda mfupi kuepuka kuleta usugu wa vimelea. Pata ushauri wa daktari
HISTOMONASI (HISTOMONIASIS)
Maelezo
   Ni ugonjwa unaosababishwa na Protozoa ambao hushambulia zaidi bata mzinga, kuku wanaweza kuwa na vimelea lakini hawaonyeshi dalili, ijapokuwa pia wanaweza kuathirika. Bata na kuku wadogo ndio wanaoathirika zaidi.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Maambukizi huenea kupitia kinyesi cha bata wagonjwa kuchafua maji na chakula, udongo, na maranda
Ø  Njia kuu ya maambukizi ni kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na Protozoa
Ø  Maambukizi yanaweza pia kupitia kwenye yai na kifaranga kuanguliwa kikiwa na ugonjwa.
Dalili
Ø  Kichwa kinageuka rangi na kuwa cheusi
Ø  Kinyesi cha njano
Ø  Kinyesi kugandamana kwenye njia ya haja
Ø  Mara nyingi vifo huwa vingi
Uchunguzi wa Mzoga
Ø  Utumbo mkubwa kuvimba na kuwa na vidonda
Ø  Utumbo mkubwa wenye rangi ya kijivu na njano, na unaweza kuwa na damu
Ø  Maini yana vidonda vya duara vyenye rangi ya njano na kijani
Ø  Uvimbe wa utandu unaozunguka utumbo iwapo vidonda vitatoboa utumbo
Tiba
Ø  Dawa aina ya Salfa kuwekwa kwenye maji au chakula. Dawa hizi ni kwa ajili ya tiba na kuzuia.
Kuzuia na Kinga
Ø  Bata mzinga na kuku watenganishwe wawe katika mabanda tofauti.
Ø  Weka utaratibu wa kuhakikisha wageni hawaingii ovyo kwenye shamba/banda
Ø  Wageni wote wachovye viatu kwenye maji yenye dawa wakati wa kuingia na kutoka shambani
Ø  Weka utaratibu madhubuti wa kupuliza dawa za viuatilifu vinavyofaa kwenye mabanda kabla ya kuingiza bata/kuku wapya
Ø  Hakikisha vyakula na maji hayachafuliwi na kinyesi
Ø  Tumia dawa za minyoo kudhibiti minyoo ya utumbo mkubwa ambayo ndiyo inayoeneza ugonjwa. Pata ushauri wa daktari.
MINYOO YA KUKU
Maelezo
   Minyoo huishi katika njia ya chakula kwenye kuku na wanyama. Minyoo inaweza kuwa na faida kwa mnyama au inaweza kuleta madhara. Minyoo mingi ya kuku husababisha madhara. Minyoo muhimu katika kuku ni aina ya Minyoo Bapa na Minyooya Duara.
MINYOO BAPA (TAPE WORM INFESTATION)
Maelezo
    Ni ugonjwa unaosababishwa na Minyoo Bapa ambayo hushambulia kuku, kanga na njiwa. Minyoo huathiri kuku na ndege wadogo na wakubwa ijapokuwa ndege wadogo wanaathirika zaidi.
Jinsi Ugonjwa Unavyoenea
Ø  Maambukizi huenea kupitia kinyesi cha kuku, ndege na wadudu wa kati (minyoo ya kwenye udongo,
kombamwiko, na panzi).
Ø  Njia kuu ya maambukizi ni kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na wadudu wa kati wanaoneza
minyoo.
Dalili
Ø  Minyoo bapa (tegu) huishi tumboni na huweza kuziba utumbo na kusababisha kifo
Ø  Kuku kukonda na kutokukua vizuri
Ø  Kuku wanaonyesha ukosefu wa damu – macho na ndimi na sehemu zisizo na manyoya hupauka
Ø  Kuhara damu
Ø  Kwa kawaida vifo huwa vingi
Tiba
Ø  Dawa za Minyoo – huwekwa kwenye maji au chakula.
Ø  Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga
Ø  Mabanda yajengwe na wavu kuzuia wadudu kuingia.
Ø  Pulizia dawa za kuua wadudu kwenye mabanda
Ø  Kinyesi cha kuku kikusanywe mara kwa mara na kusambazwa juani ili kikauke na kuua lava.

 

    Itaendelea…. 

[ad_2]

Source link

Leave a Reply