Na Augustino Chengula

Ugonjwa wa kutupa mimba (Brucellosis) ni ugonjwa unaosababishwa na vimlea vya bakteria wajulikano kitaalamu kama Brucella. Ugonjwa wa kutupa mimba ni ugonjwa muhimu kwa wanyama kwani husababisha upotevu mkubwa wa uzaliananji wa mifugo na unaweza kumuabukiza binadamu. Ugonjwa huu wa kutupa mimba huwapata wanyama wa aina mbambali ukisababishwa na Brucella abortus kwa ng’ombe, B. melitensis au B. ovis kwa mbuzi na kondoo, B. suis kwa nguruwe na B. canis kwa mbwa. Dalili zaake kubwa ni pamoja na utupaji mimba kwa asilimia kubwa, vidonda kwenye kondo la uzazi (placenta), vidona kwenye mirija ya uzazi ya ng’ombe dume na sehemu nyingine za mfumo wa uzazi. Hizi ndizo dalili kuu zinazotambulisha uwepo wa ugonjwa huu, dalili nyingine pia zipo.

Madhara makubwa ni ya kiuchumu; vifo mara chache isipokuwa kutupa mimba na vifo vya ndama wadogo kabisa. Baadhi ya wadudu hawa huendelea kuwepo kwenye hifadhi na mbuga za wanyama wakishambulia wanyama hawa bila kuonyesha madhara. Ugonjwa huu kwa binadamu unaweza kusababisha homa ya kawaida, ya kati au kali na yenye kudumu kwa muda mrefu ikishambulia viungo mbalimbali vya mwili. Maambukizi mengi yanasababishwa na kugusana na wanyama wenye ugonjwa au kula mazao ya mifugo ambao wadudu hawaja uawa vema.

Maambukizi kati ya mnyama na mnyama hutokea kwa mnyama kugusa kondo la nyuma (placenta), mimba iliyotupwa, maji maji ya mimba iliyotupwa kwa ugnjwa na maji maji toka kwenye sehemu za uzazi za ng’ombe jike. Mifugo huwa na uwezo wa kuambukiza ng’ombe wenzake ama mara baada ya kutupa mimba au anapokaribia kuzaa. Wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo mara nyingi hawaonyeshi dalili yeyote mara baada ya kutupa mimba, wanaendelea kuwa waenezaji wa ugonjwa na kuendelea kusambaza wadudu kupitia maziwa, na na maji maji yanayotoka sehemu za mfumo wa uzazi wa mimba zinazofuatia.

Maambukizi humwingia mnyama mwingine kupitia mdomoni, ngozi yenye uwazi au yenye vidonda. Bakteria wengi wa ugonjwa huu wanapatikana kwenye mbegu za ng’ombe dume ambao huendelea kukaa na wadudu na kusambaza wadudu hawa kwenye mazingira kwa muda mrefu au wakati anapanda ng’ombe jike.

 

Dalili za ugonjwa wa kutupa mimba

Kwa wanyama

Muda halisi wa kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu kwa kwa wanyama inatofautiana kati ya aina ya mnyama na umri wa mimba.

Ng’ombe: Kutupa mimba, kuzaliwa kwa ndama ambao umri haujatimia, kuzaliwa kwa ndama dhaifu, kondo la nyuma kubaki ndani; mara nyingi kutupa mimba hutokea nusu ya pili ya kipindi cha mimba. Mara baada ya kutupa mimba mara ya kwanza, mimba zinazofuata huwa hazina tatizo; lakini ng’ombe huendelea kusamabaza bakteria kupitia maziwa au majimaji ya sehemu za uzazi. Ng’ombe dume mirija ya uzazi na viungo vingine vya uzazi huwa na vidonda na majipu baadhi ya maeneo. Ugumba pia hutokea kwa jinsia zote kwa sababu ya kushambulia mifumo ya uzazi.

Mbuzi na kondoo: Bakteria husababisha kutupa mimba, kuzaliwa kwa ndama ambao umri haujatimia, kuzaliwa kwa ndama dhaifu, kondo la nyuma kubaki ndani; mara nyingi kutupa mimba hutokea nusu ya pili ya kipindi cha mimba. Mbuzi na kondoo hutupa mimba mara moja tu, uzao unaofuatia huwa kawaida. Lakini mashambulizi kwenye mfumo wa uzazi yanaweza kujirudia, utoaji maziwa hupungu ila ugonjwa wa kiwele hautokei. Mbuzi na kondoo dume mfumo wao wa uzazi mfano mirija ya kupitishia mbegu inaweza kuathirika na kupelekea kupoteza uwezo wa kuzalisha. Mbuzi na kondoo wasio na mimba hawaonyeshi dalili lakini huendelea kusambaza ugonjwa.

Kwa binadamu

Muda halisi wa kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu kwa binadamu inakadiriwa kuwa ni kati ya siku tano hadi miezi miwili na mara nyingi ni wiki mbili.

Dalili kuu za ugonjwa wa kutupa mimba huanza na maumivu makali, yenye dalili mfano wa dalili za mafua kama homa, kuuma kichwa, uchovu, maumivu ya mgongo na maumivu ya mwili mzima. Kutoka jasho jingi wakati wa usiku, kuvimba kwa ini, kongosho, kukohoa, na maumivu ya kifua. Dalili za mfumo wat umbo kama kukosa hamu ya kula, kichefuchefu, kutapika, kuharisha na kukosa choo. Dalili hizi huweza kuonekana kwa muda wiki mbili hadi nne kisha hupoteza zenyewe. Wengine huwa na homa mara kwa mara zinazokuja na kupotea kati ya siku 2 hadi 14 na wengi hupona kabisa ndani ya miezi 3 hadi 12.

 

Utambuzi wa ugonjwa

Si rahisi kutambua ugonjwa huu kwa kutumia dalili maana yapo magonjwa mengi yenye dalili hizo. Hivyo utambuzi kamili hufanyika kwa kutumia njia za kisayansi mfano kwa kutumia vipimo vinavyohusisha seramu na kuotesha wadudu maabara na kuangalia kwa kutumia darubini.

 

Matibabu na uzuiaji wa maambukizi

Kwa wanyama: Hakuna dawa iliyoonyesha ufanisi wa kutibu ugonjwa huu kwa ng’ombe au nguruwe, matibabu ya muda mrefu na antibiotics yameonyesha mafanikio kwa mbwa na baadhi ya kondoo dume tu. Maambukizi yanaweza kuzuiwa kwa kutumia madume yanayotoka kwenye shamba lisilo na ugonjwa. Kabla ya kuingiza wanyama wapya kwenye shamba ni vema kuwatenga na kuwapima kabla ya kuchanganya na wengine. Chanjo (S19 na RB51) kwa ajili ya ugonjwa huu zipo kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Kwa binadamu: Ugonjwa huu kwa binadamu unatibika kwa kutumia antibiotics, matibabu ya muda mrefu yatahitajika kuwaondoa wadudu wote. Ugonjwa huu kwa binadamu unazuilika kwa kuzuia kwa wanyama, kunywa maziwa yaliyochemshwa vizuri, kula nyama iliyopikwa vizuri, umakini na usafi wakati wa kukamua au kuchinja wanyama.

Leave a Reply