Na Augustino Chengula

Haya ni magonjwa mawili tofauti yanayoshamulia kuku yenye kufanana kwa asilimia kubwa sana. Magonjwa yote yanasababishwa na bacteria aina ya Salmonela wakitofautiana kidogo wadudu wake. Wakati Taifoidi ya kuku ikiwa inasababishwa na Salmonella gallinarum wakati ule wa pullorum ukiwa unababishwa na wadudu wajulikanao kitaalamu kama Salmonella pullorum. Magonjwa yote haya mawili yanasababisha kushuka kwa uzalishaji wa kuku na kufanya wafugaji kupata hasara kubwa sana hasa kwa kuku wa kisasa (nyama na mayai). Kwa kawaida kuku ndio wanaoathirika zaidi na magonjwa haya, lakini ndege wengine pia hupata kama bata, njiwa, kanga na mbuni. Maambukizi yake ni asilimia 10 hadi 80 hivi na vifo huongezeka kutegemea na kushuka kwa kinga ya kuku hadi kufikia asilimia 100. Vifaranga wanaweza kufa mapema mara baada ya kuanguliwa bila kuonyesha dalili yeyote ile. Mlipuko mkali hutokea kuku wakiwa bado chini ya umri wa wiki tatu ambapo vifo vinaweza kufikia asilimia 90 kama matibabu hayajafanyika kwa wakati. Wanaosalimika huwa wamedhoofika sana na wenye sura isiyovutia.
Uenezwaji
Njia kuu ya uenezaji ya moja kwa moja kwa magonjwa haya ni kupitia mayai, lakini njia nyingine ni;
-Kuku-kuku: hapa kuku mmoja hueneza ugonjwa kwa mwingine kwa kugusana
-Kuku-mayai-vifaranga: hapa kuku aliyepona ugonjwa huambukiza mayai ambapo yakianguliwa huupeleka ugonjwa kwa vifaranga kwa theruthi moja
-Vifaranga-vifaranga: ugonjwa unaenea kwa njia ya kugusana kwenye kiangulia mayai (inkubeta), kwenye box wakati wa kusafirisha na sehemu wanapolala.
-Kuku kudonoa mizoga ya kuku wenye ugonjwa hasa waliotupwa ovyo, pia panya, mbwa na paka wanaweza kubeba mizoga na kupeleka kwenye shamba jingine
-Maambukizi kupitia kuku wenye vidonda
-Kwa njia ya chakula, maji na malalia yaliyochafuliwa na kinyesi cha kuku wenye wadudu wa ugonjwa
-Pia kuku wanaweza kupata ugonjwa kutoka kwenye mikono,miguu, nguo, viatu kutoka kwa wanaohudumia kuku/wageni au vifaa vyenye wadudu vya kulishia kuku,vya maji.
-Banda lilotumika awali kama lilikuwa na ugonjwa na halikusafishwa vizuri
NB: Watakaosalimika na ugonjwa wanakuwa wasambazaji wa ugonjwa kwa uzazi ujao kwani kuku hawa huwa na afya njema wakiwa na wadudu mwilini mwao. Bakteria wa ugonjwa humpata kuku kwa njia ya hewa (mfumo wa upumuaji) au kwa njia ya mfumo wa chakula.

Dalili za homa ya Matumbo ya Kuku (Fowl Typhoid)

-Kuku anapojiwa na ugonjwa huu kwa nguvu sana upanga na ndevu zake hukunjamana

-Kuku hufa ghafla japokuwa huonekana bado ana afya sana

-Ikiwa ugonjwa unamjia kwa taratibu hadi ukakomaa, upanga na ndevu hufifia na kunyauka

-Kuku huharisha kinyesi cha rangi ya njano

-Kuku hupoteza hamu ya kula, isipokuwa hunywa maji mengi

-Kuku mwenye ugonjwaa huonekana ana wasiwasi sana

-Kuku hunyong’onyea

-Kuku huinama muda mwingi wakiwa kama na usingizi, macho yamefumba
-Manyoa yaliyotimutimu (yalikaa hovyhovyo)

 

Dalili za mharo Mweupe (Pullorum au Bacillary White Diarrhoea)

  • Toka siku tatu hadi wiki mbili baada ya kupata vijidudu vya ugonjwa, vifaranga huharisha kinyesi cheupe na vingi hufa
  • Kuku wakubwa wanaotaga, hupunguza kutaga mayai ghafla na baadhi yao hufa ghafla

 

Wakipasuliwa
-Kuwepo kwa vijiuvimbe (vinundu) kwenye mapafu, ini, ukuta wa firigisi na kwenye Moyo
-Kuvimba kwa utumbo, bandama, ini, figo, mapafu yanayoweza kuwa yamejaa damu
Utambuzi wa ugonjwa
Utambuzi unaweza kufanywa kwa kutumia dalili zilizotajwa hapo juu hasa na mfugaji, lakini ili kujilidhisha kwa uwepo wa ugonjwa huu ndani ya shamba lako kabla hujachukua hatua ni vema ukatumia vipimo vya kimaabara. huko wataotesha wadudu ili waweze kuwatambua na kuthibitisha uwepo magonjwa hayo.
Matibabu
-Magonjwa haya hutibika kwa kutumia mbambali yanayoua bakteria kama Amoksilini na Tetrasaiklini yanayopunguza vifo na uenezaji. Lakini hakuna matibabu yanayoweza kuzuia kuku wasambazaji wa ugonjwa ambao huwa wamepona.
Uzuiaji wa magonjwa haya
-Kwanza unatakiwa uanze maeneo yale wanakozalisha vifaranga, ambapo ikitokea magonjwa haya yameingia maeneo hayo basi kuku wote wanapaswa kuondolewa na kuanza upya. Banda lake lisafishwe vizuri na kupulizia madawa. Hii ni kwasababu kuku wote wanaopona wataendelea kusambaza ugonjwa kwenye mayai na vifaranga vitakavyo zaliwa. Hivyo mashamba yanayozalisha vifaranga lazima yafanye uchunguzi wa mara kwa mara kuhakikisha mashamba yao hayana magonjwa haya.
-Nunua vifaranga au kuku kutoka katika mashamba ambayo yameidhinishwa na serikali kufanya kazi hiyo na ambayo hayana historia ya magonjwa haya.
-Kama unanunua mayai kwa ajili ya uanguaji, hakikisha yanatoka kwenye mashamba yasiyo na ugonjwa
-Shamba lako likipata magonjwa haya (kwa kuthibitishwa na maabara) ni vema ukaondoa kuku wote na kuanza upya ufugaji kwani hata ukitibu watakaopona wataendelea kuusambaza ugonjwa kwa kuku wengiene. Hii ndo njia pekee ya kuuondoa ugonjwa na ndo chaguo zuri.
-Kabla hujaanza ufugaji wa kuku wengine kwa kutumia banda hilohilo, ni vema ukalisafisha vizuri, fukizia dawa na kisha liache kwa muda usiopungua mwezi mmoja ndipo ulete kuku wengine.

 

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!