Kikundi cha ulinzi wa jadi kinachoundwa na wakulima maarufu kama Mwani, kinadaiwa kuvamia nyumba ya mfugaji mmoja wa jamii ya Kimasai katika kijiji cha Kambala, wilayani Mvomero, mkoa wa Morogoro na kukatakata mifugo takribani 200 wakiwamo ng’ombe, mbuzi na kondoo kwa kutumia silaha za jadi.
Anadaiwa wavamizi hao wamefikia hatua hiyo kulipiza kisasi baada ya mifugo hiyo kudaiwa kula mazao ya wakulima.
Mwandishi wa Nipashe alifika katika kijiji hicho cha Kambala na kushuhudia baadhi ya mifugo ikiwa imekufa na mingine kujeruhiwa vibaya, huku mmiliki wa mifugo hiyo Christina Nuru, akimueleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi, saa 6:00 mchana, baada ya kuvamiwa na kundi la wakulima ambao walifunga barabara na kisha kwenda nyumbani kwake kumkamata.
Alisema baada ya kukamatwa walimpeleka eneo la bondeni jirani na nyumbani kwake na kisha kuanza kumpiga maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Alisema baadhi ya wananchi hao walibaki nyumbani kwake na kuvamia zizi lake la mifugo na kuanza kuikatakata kwa kutumia mapanga.
Alisema mifugo yake siku hiyo hakuitoa kwenda machungani na kwamba madai ya kwamba aliipeleka kwenye mashamba ya wakulima si ya kweli na kuiomba serikali imsaidie kuchukua hatua kwa waliohusika.
Mfugaji huyo alidai mbali na baadhi ya mifugo kukatwakatwa, wakulima wengine waliondoka na mifugo yake kwa kutumia pikipiki ya miguu mitatu maarufu Bajaj, huku wengine wakichinja, kuchuna na kuondoka na nyama.
Diwani wa Kata ya Hembeti (Chadema), Peter Mdidi, alisema matukio hayo ya wananchi kujichukulia sheria mkononi yanatokana na uongozi wa wilaya kutotoa ushirikiano kwa wananchi kutokana na matukio hayo kujitokeza katika eneo lake mara kwa mara.
Mdidi alisema wakati mwingine mpunga hufikia hatua ya kuchanua na kuliwa na mifugo, lakini malalamiko hayo na mengine yamekuwa yakifikishwa katika mamlaka mbalimbali bila mafanikio.
NCHEMBA AENDA ENEO LA TUKIO
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, alifika eneo la tukio na kukutana na changamoto ya wananchi kususia mkutano wa kijiji ulioitishwa, kwa madai kuwa mkuu wa wilaya amechangia kuendelea kwa mgogoro huo.
Hata hivyo, baadaye hali ikarejea kuwa shwari kwa wananchi waliokuwa wameondoka kurudi kuungana na wachache waliokuwapo na kusikiliza mkutano, hivyo Nchemba kutumia fursa hiyo kuwaeleza kusikitishwa kwake na hatua ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha kulipiza kisasi na kuagiza wote waliohusika na tukio hilo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Hili suala la kulipa kisasi kwa kukata mifugo halipo kisheria, au mkakuta shamba mkalifyeka haipo kwenye sheria, si kwa mfugaji wala kwa mkulima, leo mtakata mifugo, kesho mtakatana wenyewe kwa wenyewe, serikali haitavumilia hali hii,” alisema Nchemba na kuiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama kufuatilia waliohusika na tukio hilo.
CHANZO: NIPPASHE (Picha zimeongezwa na mmiliki wa Tovuti ya Ufugaji)