Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: hatua ya tano

Farida Mkongwe Ufugaji wa samaki hatua kwa hatua: Hatua ya nne   Na Farida Mkongwe 

HATUA YA 5: UVUNAJI, USINDIKAJI  NA UHIFADHI WA SAMAKI

Katika hatua ya 4 ya mfululizo wa  makala hii ya ufugaji wa samaki ilizungumzia ulishaji na utunzaji wa samaki bwawani.

Katika hatua hiyo tuliona kuwa samaki  wanatakiwa wapewe chakula angalau mara 2 kwa siku, samaki wapewe vyakula tofauti kutegemeana na silka yao, mfugaji anatakiwa kukagua kiwango cha hewa kilichopo kwenye maji angalau mara 2 kwa wiki pia maji yanatakiwa yafanyiwe ukaguzi dhidi ya hewa chafu.

Katika hatuia hii ya 5 tunaangalia uvunaji, usindikaji na uhifadhi wa samaki. Tukianzia na suala la uvunaji hapa mtaalamu wetu wa lishe ya samaki na uzalishaji kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Wanyama SUA Dr. Berno Mnembuka anatueleza kuwa samaki wenye kufugwa wanaweza kuvunwa kwa mbinu 2 zifuatazo.

samaki 1

Mbinu ya kwanza: Mfugaji anaweza kupunguza maji kwenye bwawa ili samaki waweze kuvuliwa kiurahisi lakini kutokana na uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali ya kufugia.

Mbinu ya pili:  Mfugaji anaweza kuvua samaki kwa kutumia nyavu. Iwapo mfugaji atatumia mbinu hii ya pili basi ni vema akapata ushauri wa wataalamu kuhusu ukubwa wa macho ya nyavu ya kuvulia.

Dr. Mnembuka anasema kuwa mfugaji asipozingatia suala la nyavu yenye macho muafaka katika uvunaji wake basi athari zake ni uchafuzi wa maji pamoja na kukokoa vifaranga pamoja na mayai hali ambayo itaathiri uzalishaji wa samaki katika mzunguko utakaofuata.

Tukizungumzia upande wa usindikaji na uhifadhi tunafahamu kuwa samaki ni miongoni mwa mazao yanayoharibika haraka hivyo basi mfugaji na hata muuzaji ni vizuri wakazijua mbinu muafaka za usindikaji na uhifadhi wa samaki.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe ya samaki na uzalishaji Dr. Mnembuka, zipo mbinu mbalimbali za usindikaji na uhifadhi wa samaki, mbinu mojawapo ni kutumia chumvi, chumvi hiyo inaweza ikawa kavu ambayo utaweka kwenye chombo utakachohifadhia samaki kisha utawaweka samaki wenyewe na baadaye utanyunyizia tena chumvi juu ya hao samaki, hapo samaki wanaweza kukaa muda wa saa 24 bila kuharibika.

Pia unaweza kutumia rojo rojo ya chumvi, unaweza kuchukua chumvi ukaiweka kwenye maji unakoroga kisha unachukua samaki unawaweka kwenye ile rojo rojo ya chumvi.

Mbinu ya pili ya uhifadhi wa samaki ni kutumia moshi, unaweza kutumia moshi baridi ambapo chanzo cha moshi huo kinakuwa mbali na chemba cha kukaushia samaki kinachofanyika ni kuusafirisha ule moshi kwa njia ya bomba hadi pale kwenye eneo la kukaushia samaki ambapo ule moshi utanyonya unyevunyevu uliopo kwenye samaki na kuwaacha wakavu hivyo hawawezi kuharibika kwa haraka au unaweza kutumia moshi wa joto ambao unakuwa karibu na chemba cha kukaushia.

Mbinu nyingine ni kukaanga samaki kwenye mafuta, kwa mujibu wa mtaalamu wetu njia hii siyo nzuri sana ukilinganisha na nyingine kwa sababu samaki ni zao lenye mafuta hivyo ukiwaakaanga utakuwa unawaongezea mafuta zaidi.

Mbinu nyingine ni kuwagandisha samaki kwenye barafu, unaweza kuwagandisha samaki ukiwa umewakata vipande (minofu) au hata wazima wazima kwa maana ya kutowakata.

Pia unaweza kuwahifadhi samaki kwa kutumia njia ya uvundikaji, njia hii hatumiki sana kwa sababu mara nyingi samaki wanaofaa kuwavundika ni nguru, wataalamu mbalimbali wamefanya utafiti wakagundua kuwa samaki anayefaa kwa kuvundikwa ni nguru ukitumia njia hii kwa samaki wengine wanaharibika.

Hadi kufikia hapo ndiyo tunahitimisha hatua hii ya 5 ya ufugaji wa samaki, usikose kufuatilia hatua ya 6 ambayo itakuwa ikizungumzia masoko ya samaki.

 

CHANZO: SUAMEDIA

Leave a Reply

error: Alert: Imezuiliwa !!