Kuhifadhi mbegu za samaki kwa mzunguko mwingine
Unapovuna samaki, hakikisha kuwa vifaranga au samaki wazazi utakaokuwa umewachagua wanawekwa katika kijibwawa kingine (kinachojulikana kama nursery pond) kabla ya kuwarudisha bwawa la kukuzia (production pond). Ni muhimu kufanyia bwawa matengenezo na kulijaza maji kabla ya kuweka samaki tena. Hili ni muhimu kwa mfugaji kwani kinamhakikishia mfugaji kujua kuwa anapanda mbegu changa na ambao hawajadumaa. Pia humhakikishia kujua kuwa samaki waliopandwa wanalingana na ujazo wa bwawa, yaani vifaranga viwili kwa kila mita moja ya mraba na pia hurahisisha maji ya bwawa kurutubika kirahisi.
Uzalishaji wa vifaranga bora
Chagua samaki wazazi wazuri kulingana na umbile lao kama rangi, ukubwa, afya na sura zao. Samaki hawa watengwe na wale wasio na sifa hizo na wasiruhusiwe kuzaliana nao. Mfugaji anaweza kununua wazazi hawa kutoka katika chanzo kinachofahamika kuwa kina samaki bora. Dhibiti ubora wa samaki hawa wazazi kwa kutoruhusu miingiliano na samaki wenye ubora hafifu. Chuja vema maji yanayoingia bwawa. Ikiwezekana, tumia samaki wenye ukubwa wa zaidi ya gramu 100. Hii itakuwezesha kutenganisha wazazi kutoka kwa vifaranga kila baada ya kuzaliwa (reproduction cycle).
Endelea kuwatumia wazazi hawa kila unapohitaji vifaranga kutegemeana na jinsi wanavyoendelea kuzaa vifaranga bora. Pamoja na ubora wa wazazi hawa, kuna umuhimu wa kuchagua na kuwaondoa vifaranga wasio kuwa na ubora unaohitajika au ambao ubora wao unatiliwa mashaka (culling).
Ni muhimu mfugaji afahamu uzuri wa kutumia vifaranga bora. Kausha bwawa kabisa angalau mara moja kila baada ya miezi sita hadi nane ili kuondokana na samaki wasio na ubora unao hitajika, kuua maadui wa samaki na kuondokana na hali ya kuwa na samaki wengi kwenye bwawa zaidi ya kiwango kinachotakiwa na pia hali ya samaki kuzaliana kinasaba “inbreeding”. “Culling na grading” ni muhimu kuanza baada ya siku 30 hadi 45 baada ya samaki wakubwa kuwa wamewekwa kwenye bwawa na hufanyika kwa kutumia kawavu kadogo ambacho kina matundu madogo.
Endelea kufanya kazi hii kila baada ya wiki mbili hadi nne.
Chanzo: Blogu ya ufugaji bora wa samaki