Ufugaji wa kuku wa mayai hatua kwa hatua: hatua ya saba

-Kinga dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu

Katika hatua hii nitaelezea magonjwa muhimu yanayo wakabili kuku wa mayai na wadudu walibifu na namna ya kukabiliana navyo. Ni hatua muhimu sana kwa mufugaji ili kuhakikisha unapunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa kuku au kuongeza uzalishaji wa mayai. Magonjwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wafugaji wengi n ahata kufanya wengine waogope kuingia kwenye ufugaji wa kuku wa mayai. Wafugaji wengi pia hushindwa kujua wapi pa kuanzia ili kukabiliana na kadhia hii inayowapelekea hasara kubwa. Wengi wamepoteza mitaji mikubwa kutoka kwenye fedha zao au fedha walizokopa kwenye mabenki au vikundi. Hivyo ni muhimu sana kwako mfugaji au unayetaka kuanza ufugaji wa kuku wa mayai kufuatilia elimu hii kwa makini na kuchukua hatua. “Kinga ni bora kuliko tiba” ndiyo kauli itakayofungua wapi pa kuanzia kwenye hatua hii ya kupambana dhidi ya magonjwa. Tiba inatakiwa iwe ni hatua ya mwisho kufikiria unapotaka kuzuia magonjwa kwenye kuku wako hasa pale kinga inapokuwa imeshindwa.

 

Kuzuia maambukizi ya magonjwa

Ili kuweza kuzuia maambuki ya magonjwa kwenye mifugo yako ni muhimu sana kujua namna magonjwa hayo yanavyoweza kuwafikia kuku wako au namna kuku wako wanavyoweza kupata magojwa. Kuku wako wa mayai anaweza kupata vimelea vya wadudu wa magonjwa na hatimaye kuwa mgonjwa kwa njia zifuatazo:

 

(i). Maambukizi ya kuku-kwa-kuku kupitia kugusana, kugusa kinyesi chenye wadudu wa magonjwa,

-Ili kuzuia ueneaji wa magonjwa kwa njia hii mfugaji unapaswa kwanza kuhakikisha kuwa kuku wako wa mwanzo/vifaranga unapata kutoka kwenye shamba linaloaminika. Shamba linalofuata taratibu za kuzuia magonjwa kwa vifaranga ikiwa ni pamoja kuchanja vifaranga wa siku moja dhidi ya ugonjwa wa Mahepe (Marek’s disease). Baada ya kuwa na vifaranga wasio na ugonjwa hakikisha banda lako la kuku linakuwa safi hasa kama unafugia sakafuni. Kama unafanya ufugaji wa vizimba (cages) ambao ndo unashauriwa kwa kuku wa mayai ili kukabiliana na maabukizi tatizo huwa si kubwa sana kwani kinyesi cha kuku mmoja hakimfikii kuku mwingine. Hata swala la kukugusana kuku kwa kuku huwa halipo pia.

 

(ii). Kupitia maambukizi toka kwa watu wanaotembelea shamba lako la kuku au wanaolisha kuku wako,

-Hakikisha watu wanaotembelea shamba lako ni wachache na kama ni lazima kuingia kwenye banda la kuku. Pia weka dawa ya kuzuia maambukizi ya vimelea vya magonjwa mlangoni mwa banda ili watu wakanyage dawa kabla ya kuingia ndani y abanda. Mtu anayelisha kuku wako asiwe na nafasi ya kuingia kwenye mabanda ya wafugaji wengine.

 

(iii). Kupitia vifaa, chakula au mazingira yenye vimelea vya magonjwa,

-Hakikisha vifaa vya chakula na maji vinaoshwa mara kwa mara na kutunzwa mahali pazuri na mazingira yanayozunguka banda lako yawe safi. Chakula unachowapa kuku wako hakikisha unakipata kwenye chanzo chenye uhakika wa kutokuwa na vimelea vya magonjwa. Chakula kihifadhiwa mahali safi pasipo na unyevu ili kuzuia sumu kuvu yenye madhara kwa kuku. Chanzo cha maji unayowanywesha kuku wako kisiwe na vimelea vya magonjwa kwa kuku.

 

(iv). Kupitia wanyama pori, wadudu na panya wanaoweza kuwa na vimelea vya magonjwa yanayoweza kuwapata kuku.

-Hili linapaswa kuzingatiwa wakati wa kuchagua eneo la kujenga nyumba ya kuku kwa kujenga nyumba ya kuku isiruhusu wadudu kuingia ndani ya banda. Madirisha yawekewe nyavu za kuzuia wanyama kama panya na nyoka pamoja na wadudu kama nzi, mjusi au kenge wanaoweza kuingia kula mayai. Hakikisha hakuna nyufa au mianya ya kuwaruhusu kuingia ndani. Soma zaidi SIFA ZA BANDA BORA LA KUKU.

 

Chanjo

Njia hii ni muhimu kwa kuzuia maambuzi ya vimelea vya magonjwa na kila ugonjwa una chanjo yake na haiwezi kukinga dhidi ya ugonjwa mwingine tofauti na ule ulilengwa. Hivyo ni muhimu kujua unakinga dhidi ya ugonjwa gani. Kuna magonjwa ya aina kuu mbili ambayo unaweza ukakinga kwa kutumia chanjo; yanayo enezwa na virusi na bakteria. Tena hakikisha unakinga kwa wakati na si baada ya kuku kuugua. Kuku wakisha kuwa na ugonjwa hutakiwi kuwachanja kwani kufanya hivyo ni kuwaongezea ugonjwa. Kuku wagonjwa wanatibiwa na si vinginevyo, unakuwa umechelewa.

KITABU CHA MAGONJWA MAKUU YA KUKU, TIBA NA KINGA

 

Utajuaje kuwa kuku wako ni mgonjwa?

Tumesema king ani bora kuliko tiba, lakini kuna uwezekano pia wa kushindwa kukinga au kwa sababu zilizo nje ya uwezo wako kuku wako wakaugua ugonjwa fulani. Je, utajuwaje kuwa kuwa wako ni mgonjwa? Bilas haka ni swali jepesi maana hata binadamu akiumwa unaweza kujua kuwa huyu mtu anaumwa kwa kuona dalili tofauti na akiwa mzima. Vile vile kuku nao wakiumwa huonyesha dalili za utofauti na kuku asiye mgonjwa. Kwa vile si mtaalamu wa mifugo au mtaalamu sana wa magonjwa lakini huwezi kushindwa kubaini kuwa kuku wangu ni mgonjwa. Unaweza usijue dalili zote na ukaelezea kama mtaalamu. Dalili zifuatazo za jumla kwa magonjwa mengi zitakupa mwanga kwamba kuku wangu ni mgonjwa. Kwa dalili za magonjwa na kinga kwa ugonjwa mmoja mmoja rejea kitabu hapo juu au soma zaidi UKURASA WA MAGONJWA YA KUKU NA TIBA.

 

(i). Mfumo wa chakula- Kuharisha ni dalili kwa magonjwa mengi hasa yanayoshambulia mfumo wa chakula. Mharo unaweza kuwa maji maji wenye rangi nyeupe, nyekundu (mharo damu), njano au kijani kutegemeana na ugonjwa. Mharo huo unaweza kuganda eneo la nyuma maeneo ya kutolea kinyesi na hukaukia hapo. Kuharisha hupelekea maji kupungua mwilini na hii hujionyesha zaidi kwa vifaranga.

 

(ii). Tatizo la mfumo wa hewa- Dalili za mfumo wa hewa kwa kuku mgonjwa ni pamoja na kukohoa, kupiga chafya, kuchuruzika kwa makamasi na kuvimba uso.

 

 

(ii). Dalili nyingine ni pamoja na kupungua uzito, kutokua kwa wastani, kupunguza utagaji wa mayai, kupunguza kulan a kunywa maji, manyoa yasiyo na mvuto, vifo vingi ndani ya muda mfupi au mfululizo, mtembeo usio wa kawaida na kupooza, kupinda kichwa na shingo pamoja na kunyong’onyea.

 

Uonapo dalili hizi basi wasiliana na mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe ili aweze kukusaidia kubaini tatizo na kutoa tiba sahihi.

 

Naamini umenufaika na makala hizi za ufugaji wa kuku wa mayai hatua kwa hatua na hapa tunahitimisha safari yetu ya ufugaji wa kuku wa mayai. Endelea kufuatilia makala nyingine zitakazokujia hivi punde za ufugaji wa kuku wa nyama. Pia endelea kujielimisha juu ya ufugaji wa mifugo mingine kupitia Tovuti yetu hii ya ufugaji.

Leave a Reply